Kabla hujaanzisha jumuiya, bainisha unalokusudia – je, ni kutoa taarifa kuhusu shughuli za shule, kutoa usaidizi kwa wanafunzi na walimu, kushiriki mbinu bora na nyenzo mpya za kufundishia, au kitu kingine? Lengo lako litakusaidia kubainisha wahusika utakaowajumuisha kwenye jumuiya na ni vikundi gani wataingia. Unaweza kuanzisha au kuongeza vikundi vifuatavyo:
- vikundi vya walimu kulingana na kidato au somo;
- kikundi cha wafanyakazi ambao si walimu;
- vikundi vya wanaoshughulikia miradi tofauti;
- vikundi vya wazazi kulingana na darasa au gredi;
- vikundi vya wanafunzi kulingana na darasa, vikisimamiwa na walimu;
- vikundi vya timu za michezo au shughuli nyingine za shule.
Kuwa na lengo bayana la jumuiya kutawasaidia wasimamizi na wanajumuiya kuelewa sababu za kuongezwa au kutoongezwa kwa vikundi fulani. Kwa mfano, ikiwa lengo lako ni kushiriki taarifa kuhusiana na shule, unaweza kuongeza kikundi cha wazazi wa wachezaji wa timu ya soka ya shule, ili washiriki maelezo kuhusu vifaa vya michezo na ratiba za mazoezi. Kwa upande mwingine, kikundi cha wazazi ambao lengo lao ni kupiga soga kuhusu jambo linalowavutia hakitaongezwa.
Huenda waliomo kwenye baadhi ya vikundi wakabadilika sana kila mwaka – kama vile vikundi vya darasa. Hili likifanyika, itakuwa rahisi kufunga kikundi na kuanzisha kingine kipya. Vikundi vingine, kama vile timu za michezo, vikundi vya masomo au miradi, huenda vikahitaji kuongezwa na kuondolewa mara kwa mara. Kuna uwezekano mkubwa wa kutobadilika kwa vikundi fulani kama vile muungano wa wazazi au wafanyakazi ambao si walimu, japo mara kwa mara wapo wanakikundi watakaoongezwa na wengine kuondolewa. Ikiwa vikundi vingi vinahitaji kuondolewa kila mwaka, huenda ikawa rahisi zaidi kufunga jumuiya na kuanzisha nyingine mpya.